Latest News 18 Jan 2023

News Images

Prof Mbarawa Apongeza MV Mwanza Kufikia 80% ya Ujenzi

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Makame Mbarawa (MB) amewapongeza Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kwa Utekelezaji unaoridhisha wa Mradi wa Ujenzi wa Meli ya Kisasa ya MV Mwanza inayojengwa kwa gharama ya Bilioni 108 itakapokamilika.

Prof. Mbarawa amesema hayo leo (Januari 17, 2023) alipofanya ziara kwenye bandari ya Mwanza Kusini ambapo Meli hiyo inajengwa na kukuta Ujenzi umefikia Asilimia 80 ya Utekelezaji.

Amesema Wizara hiyo imeridhika na utekelezaji wa mradi huo na akabainisha kuwa ifikapo februari 15 mwaka huu meli itaondolewa kwenye chelezo na kuingizwa kwenye Maji ambapo Ujenzi wa hatua zilizobaki utaendelea ikiwa majini.

"Ujenzi unaenda vizuri na Serikali tumeridhika na hatua zote na ifikapo tarehe 15 mwezi ujao (februari) meli hii itaingizwa kwenye Maji kwa ajili kuendelea na ujenzi wa hatua zinazofuata za ukamilishaji." Mhe. Mbarawa.

Aidha, amewaagiza Kampuni ya Huduma za Meli kufuatilia kwa kina ufungaji wa vifaa vya kumsaidia Nahodha kuweza kubaini mahali gani pana hali gani kama vile kina kidogo au miamba (Navigation Chat).

Vilevile, amewataka MSCL kusimamia Ujenzi wa Bandari ya Kemondo (Kagera) ili ikamilishwe kwa haraka na kuhakikisha anapatikana mkandarasi wa kujenga Bandari ya Mwanza kusini ili Meli hiyo ianze kazi mara moja bila kusubiri jambo lolote.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima ameipongeza Wizara hiyo kwa kazi nzuri wanazoendelea kusimamia huku akiitaja Miradi ya kimkakati ya Reli ya Kisasa, Daraja la Kigongo-Busisi na Meli hiyo ambayo yote kwa pamoja itawainua sana wananchi wa Mwanza na Tanzania kwa ujumla.

Aidha, Mhe. Malima ametoa wito kwa MSCL kujifunza kwenye Bandari kubwa za kimataifa ili kuhakikisha wanajenga bandari za kisasa zitakazoendana na Meli hiyo inayotarajiwa kuwanufaisha watanzania na nchi za jirani.